Psalms 77

Matendo Makuu Ya Mungu Yanakumbukwa

(Kwa Mwimbishaji: Mtindo Wa Yeduthuni. Zaburi Ya Asafu)


1 aNilimlilia Mungu ili anisaidie,
nilimlilia Mungu ili anisikie.

2 bNilipokuwa katika taabu, nilimtafuta Bwana,
usiku nilinyoosha mikono bila kuchoka
na nafsi yangu ilikataa kufarijika.


3 cEe Mungu, nilikukumbuka wewe, nikalia kwa huzuni;
nikatafakari, roho yangu ikadhoofika.

4 dUlizuia macho yangu kufumba;
nilikuwa nasumbuka, nikashindwa kusema.

5 eNilitafakari juu ya siku zilizopita,
miaka mingi iliyopita,

6 nilikumbuka nilivyoimba nyimbo usiku.
Moyo wangu ulitafakari
na roho yangu ikauliza:


7 f“Je, Bwana atakataa milele?
Je, hatatenda mema tena?

8 gJe, upendo wake usio na mwisho umetoweka milele?
Je, ahadi yake imekoma nyakati zote?

9 hJe, Mungu amesahau kuwa na huruma?
Je, katika hasira amezuia huruma yake?”


10 iNdipo nikawaza, “Huu ndio udhaifu wangu:
lakini nitakumbuka
miaka ya mkono wa kuume
wa Aliye Juu Sana.”

11 jNitayakumbuka matendo ya Bwana;
naam, nitaikumbuka miujiza yako ya zamani.

12 kNitazitafakari kazi zako zote
na kuyawaza matendo yako makuu.


13 lEe Mungu, njia zako ni takatifu.
Ni mungu yupi aliye mkuu kama Mungu wetu?

14 mWewe ndiwe Mungu utendaye miujiza,
umeonyesha uwezo wako katikati ya mataifa.

15 nKwa mkono wako wenye nguvu umewakomboa watu wako,
uzao wa Yakobo na Yusufu.


16 oMaji yalikuona, Ee Mungu,
maji yalikuona yakakimbia,
vilindi vilitetemeka.

17 pMawingu yalimwaga maji,
mbingu zikatoa ngurumo kwa radi,
mishale yako ikametameta huku na huko.

18 qNgurumo yako ilisikika katika upepo wa kisulisuli,
umeme wako wa radi ukaangaza dunia,
nchi ikatetemeka na kutikisika.

19 rNjia yako ilipita baharini,
mapito yako kwenye maji makuu,
ingawa nyayo zako hazikuonekana.


20 sUliongoza watu wako kama kundi
kwa mkono wa Musa na Haruni.
Copyright information for SwhKC